IQNA

Nchi 93 Kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran

10:13 - November 30, 2017
Habari ID: 3471288
TEHRAN (IQNA)-Mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umepangwa kufanyika wiki ijayo katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran kwa kuhudhuriwa na wageni 300 kutoka nchi 93 duniani.

Akizungumza na waandishi habari Jumatano mjini Tehran, Ayatullah Muhsin Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mkutano huo ambao utafanyika kuanziaDisemba 5-7 utawaleta pamoja wanazuoni, wanafikra na viongozi wa kisiasa kutoka nchi za Kiislamu wakiwemo mawaziri kadhaa. Aidha amesema miongoni mwa washiriki pia kutakuwemo wanazuoni 220 wa Kishia na Kisunni kutoa ndani ya Iran.

Amesema kiwango cha ushiriki katika mkutano huo ni ishara kuwa ulimwengu wa Kiislamu una azma ya kukabiliana na madola ya kibeberu na kiistikbari na kuzima njama zao za kuibua mifarakano.

Ayatullah Araki amesema mada kuu ya mkutano wa mwaka hii ni "Umoja na Mahitajio ya Ustarabu Mpya wa Kiislamu."

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3668177

captcha