IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani, Israel na vibaraka wao Mashariki ya Kati ni mafirauni wa zama hizi

19:51 - December 06, 2017
Habari ID: 3471298
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani, utawala haramu wa Israel, wenye fikra mgando na wategemezi wa madola makubwa ni mafirauni wa zama hizi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhammad saw na mjukuu wake Imam Ja'afar Swadiq as alipokutana na Wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola, maafisa wa mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu walioko hapa mjini Tehran na wageni walioshiriki katika mkutano wa Umoja wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa, baadhi ya wanasiasa wa Kimarekani wamekiri bayana kwamba, kuna ulazima wa kutokea vita na machafuko magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) ili utawala ghasibu wa Israel uwe katika amani na wakati huo huo kuufanya ulimwengu uliotapakaa damu wa Kiislamu usipate maendeleo.

Aidha alielezea masikitiko yake makubwa kutokana na baadhi ya watawala wa nchi za Mashariki ya Kati kufuata kibubusa matakwa ya Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia wala shauku ya kuwa na hitilafu na madola ya Kiislamu na kwamba, kama ambavyo ndani ya Iran kuna umoja na udugu unaotawala, inaamini kuwa, katika Ulimwengu wa Kiislamu pia kuna udharura wa kuweko umoja na mshikamano na imekuwa ikifuatilia jambo hilo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, “Lugha yetu kwa wanaoifuata Marekani katika eneo hili ni lugha ya nasaha na tunawausia wahusika kwamba, kuwahudumia madhalimu wa dunia ni kwa madhara yao wenyewe na kama inayovyoeleza Qur'ani, kuwa pamoja na madhalimu hakuna hatima nyingine ghairi ya kuangamia.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema kuwa, lengo la mwisho la maadui ni kuanzisha makundi ya kitakfiri, kuanzisha vita baina ya Shia na Suni. Amesema, tiba ya machungu na maumivu ya Ulimwengu wa Kiislamu na kufikia katika nguvu na heshima ni kudumisha umoja wa Kiislamu na kusimama kidete mbele ya Uzayuni na maadui wengine wa Uislamu.

Kuhusiana na kadhia ya Quds Tukufu (Jerusalem), Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Madai ya maadui wa Uislamu kuhusu kutangazwa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, yanatokana na kushindwa kwao na bila shaka ulimwengu wa Kiislamu utakabiliana vilivyo na njama hiyo na  Wazayuni kupata pigo kubwa zaidi, ambapo bila shaka hatimaye Palestina itakombolewa.

3669934

captcha