IQNA

Mashindano ya Qur'ani ya Malaysia yamalizika, Binti Mtanzania nafasi ya tatu

17:30 - May 13, 2018
Habari ID: 3471510
KUALA LUMPUR (IQNA) – Washindi wa Mashindano ya 60 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Malaysia wametangazwa leo Jumapili

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA katika mashindano hayo, majina ya washindi yalitangazwa katika sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Putra World Trade Center mjini Kuala Lumpur na kuhudhuriwa na Mfalme wa Malaysia.

Kwa mujibu wa maamuzi ya jopo la majaji wa mashindano hayo, mshindi katika kategoria ya Qiraa ya Qur'ani Tukufu kitengo cha wanaume alikuwa ni Abdullah bin Fahmi wa Malaysia akifuatiwa na Mukhtar Dehqan wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na Salahuddin Haysam wa Algeria.

Katika kategoria ya wanaume ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu, nafasi ya kwanza imechukuliwa na Kalim Sidiqi wa Bangladesh akifuatiwa na Walid Hammad Muhammad Marzuqi wa Umoja wa Falme za Kiarabu huku mshiriki wa Sudan akichukua nafasi ya tatu.

Katika kitengo cha wanawake, mshindi wa kategoria ya Qiraa alikuwa ni mshiriki wa Malaysia akifuatiwa na wawkilishi wa Indonesia na Singapore kwa taratibu. Halikadhalika katika kitengo cha wanawake katika kategoria ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu nafasi za kwanza hadi tatu kwa taratibu zimechukuliwa na wawakilishi wa Mauritania, Malaysia na Bi Ashura Amani Lilanga wa Tanzania. Itakumbukwa kuwa Bi. Amani alishika nafasi ya tatu pia katika Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyofanyika mjini Tehran hivi karibuni.

Mashindano hayo ya 60 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Malaysia yalianza Jumatati na yalikuwa na washiriki kutoka nchi 56.

3713722

captcha