IQNA

Msomi wa Kuwait asema Saudia imebadilisha Msikiti wa Makka kuwa jumba la makumbusho

21:41 - June 25, 2020
Habari ID: 3472898
TEHRAN (IQNA) – Msomi na mhadhiri wa chuo kikuu nchini Kuwait ameibua utata katika mitandao ya kijamii baada ya kusema hatua ya Saudia wa kupunguza idadi ya mahujaji mwaka huu itaubadilisha Msikiti Mtakatifu wa Makka, Al Masjid al Haram, kuwa sawa na jumba la makumbusho.

Hakim al-Mutairi mhadhiri wa Tafsiri ya Qur’ani Tukufu na Hadithi katika Chuo Kikuu cha Kuwait amekasirishwa na uamuzi wa Saudia wa kuwazuia mahujaji kutoka nje ya Saudia kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.  Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema: “Hii Hija itakuwa ni urasimu tu na Msikiti Mtakatifu wa Makka umebadilishwa kuwa jumba la makumbusho ambapo watakaohiji ni wale tu walioidhinishwa na utawala wa Saudia. Hii si Hija ambayo Mwenyezi Mungu SWT ameitaja katika aya ya 27 ya Suratul Hajj ifuatavyo: Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.”

Al-Mutairi katika sehemu nyingine ya ujumbe wake wa Twitter amesema kuwa, “Mwenyezi Mungu ameujalia Msikiti Mtakatifu wa Makka kuwa sehemu ya Hija na hakuna mwenye haki ya kuwazuia Waislamu kuhiji wawe wanaishi karibu na msikiti huo au wanatoka sehemu za mbali.”

 Akifafanua kuhusu nukta hiyo ameashiria aya ya 25 ya Suratul Hajj isemayo: Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu.”

Msomi wa Kuwait asema Saudia imebadilisha Msikiti wa Makka kuwa jumba la makumbusho

Ujumbe wa Al-Mutairi umeibua gumzo katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimuunga mkono kikamilifu na wengine wakimpinga.

Saudia ilitangaza Jumatatu kuwa ni watu wachache sana watakaoruhusiwa kuhiji mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imesema kuwa, Hija ya mwaka huu itashirikisha idadi ndogo ya mahujaji ambao ni raia wa Saudia na raia wa kigeni ambao ni wakazi wa nchi hiyo. Hatua hiyo ya kuwazuia mahujaji kutoka nje ya Saudia imechukuliwa kutokana  kile wakuu wa ufalme huo wametaja kuwa ni kuendelea maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

3906857

captcha