IQNA

Mwanae Sheikh Zakzaky

Serikali ya Nigeria imeendelea kufanya vitendo vya ukandamizaji dhidi ya Sheikh Zakzaky

23:10 - July 01, 2020
Habari ID: 3472920
TEHRAN (IQNA) - Mtoto wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali ya Rais Buhari imeendelea kufanya vitendo vya ukandamizaji dhidi ya baba yake huyo anayeshikiliwa gerezani.

Muhammad Ibrahim Zakzaky akizungumzia jinai zilizofanywa na serikali ya Nigeria dhidi ya familia yake na Harakati yay Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo imewaua watoto sita wa Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Kuhusiana na afya ya Sheikh Zakzaky, Muhammad Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, hali ya kiafya ya baba yake bado hairidhishi na kwamba, uwezo wake wa kuona unapungua siku baada ya siku.

Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.

Makumi ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na kiongozi huyo wa harakati hiyo wamewekwa kizuizini tangu walipotiwa nguvuni mwaka 2015 baada ya jeshi la Nigeria kushambulia Husainia ya mji wa Zaria jimboni Kaduna; na tangu wakati huo hadi sasa wanaendelea kusota jela pasi na kuthibitishiwa makosa na mashtaka yanayowakabili.

Mahakama Kuu ya Nigeria iliwahi kutoa hukumu iliyosisitiza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe hawana hatia yoyote na ikaamuru waachiliwe huru, lakini wawili hao wangali wanaendelea kuwekwa jela na hivi sasa hali zao za afya ni mbaya sana.

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky, 66, na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kushambulia Hussainiyah iliyoko katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria wasiopungua 1,000, wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi. Sheikh Zakzaky na mke wake walipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na askari wa Nigeria katika tukio hilo.

 

3907679

captcha