IQNA

Maandamano makubwa ya Wapalestina katika 'Siku ya Hasira'

15:49 - July 02, 2020
Habari ID: 3472923
TEHRAN (IQNA) - Jumatano Wapalestina walifanya maandamano makubwa dhidi ya utawala haramu wa Israel chini ya anuani ya ‘Siku ya Hasira’ maandamano ambayo yaliungwa mkono kimataifa.

Jumuiya na asasi 16 za Palestina na za kimataifa zilitoa wito wa kufanyika maandamano hayo. Watumiaji wa mitandao ya kijamii nao walishiriki kwa kuweka jumbe mbalimbali kama #hapana-kutwaa, #hapana-kupora na kadhalika, na hivyo kuonyesha upinzani wao kwa mpango wa Israel wa kutaka kupora ardhi zaidi za Wapalestina.

Kufuatia upinzani mkali wa Palestina na kuongezeka malalamiko na indhari katika uga wa kimataifa hatimaye kumemlazimisha Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel aakhirishe mpango wake wa kutwaa ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina na sasa mpango huo utatekelezwa wakati mwingine.

Mwezi Aprili mwaka huu, Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, walifikia makubaliano ya kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina. Mpango huo ulipangwa kuanza kutekelezwa jana tarehe Mosi Julai. Netanyahu alikuwa akikazania mno kutekelezwa mpango huo katika tarehe iliyokuwa imeafikiwa hapo kabla. Hata hivyo, mashinikizo yamemlazimisha asogeze mbele utekelezaji wake.

Jumatatu, Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, mpango wa Israel wa kupora ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na kuitaka Tel Aviv iachane na mpango huo.

3471860

captcha