IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran

Leo Wazayuni wamezingirwa na wanamapambano wa Palestina, Lebanon, Iraq na Yemen

18:28 - May 06, 2022
Habari ID: 3475212
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umezingirwa na wanamapambano wa Kiislamu walioko Palestina, Lebanon, Iraq na Yemen.

Hujjatul-Islam Walmuslimin Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi-Fard amesema kuwa, hii leo Palestina ndiyo suala nambari moja katika Ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Licha ya vizingiti visivyo vya kibinadamu na vituo vya upekuzi mkali, zaidi ya Waislamu laki mbili wa Kipalestina wameshiriki katika Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) -unaokaliwa kwa mabavu na Israel-, na jambo hili linatia matumaini makubwa na kuwavunja moyo maadui wa Uislamu."

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ameeleza kuwa awali utawala wa Kizayuni ulikuwa katika hali ya kuhujumu na kwamba vita vya sita ni kielelezo cha hali hiyo na kuongeza kuwa: Katika vita hivyo nchi tatu za Misri, Syria na Jordan zilishambuliwa na Wazayuni, lakini leo hii utawala huo umebadilisha nafasi yake kutoka kwenye hali ya kuhujumu na kwenda kwenye hali ya kujihami mbele ya mashambulio na vipigo vya wanamuqawama. 

Hujjatul-Islam Walmuslimin Abu Turabi-Fard amesisitiza kuwa: Leo hii Wazayuni wamezingirwa wa wanamapambano huko Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kutoka kwa Hizbullah huko Lebanon, al Hashdu al Shaabi nchini Iraq na wapiganaji shupavu wa Yemen, na hali ya mambo ni tofauti kabisa. Hatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesisitiza kuwa, hali hii itaendelea hadi utawala wa Kizayuni wa Israel utakapoangamiza kikamilifu.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria maandamano makubwa ya Ijumaa iliyopita dhidi ya Wazayuni na kueleza kuwa, Ijumaa iliyopita Umma wa Kiislamu ulihudhuria kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Amesema vyombo vya habari vya dunia vimekiri ukweli kwamba, maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika Ramadhani ya mwaka huu kwenye Ulimwengu wa Kiislamu yalikuwa na utukufu maalumu na yametoa bishara njema ya umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu kwa ajili ya kulinda na kuitetea ardhi ya Quds Tukufu. 

4054954

captcha