IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kufungamana na Qur'ani kunaimarisha jamii ya Kiislamu

18:28 - June 30, 2014
Habari ID: 1424379
Katika siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ugeni wa Allah Karima ambao pia ni machipuo ya Qur'ani, idadi ya wasomaji bora wa tajwidi, maustadhi na mahafidhi wa Kitabu cha Allah SWT, jana mjini Tehran walishiriki katika kikao na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwenye mahafali ya kufungamana na Qur'ani.

Vikundi mbali mbali vya kusoma tajwidi kwa pamoja, navyo vilikuwepo kwenye mahafali hiyo na vimesoma aya za Qur'ani Tukufu za kumshukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu Azza Wajalla.
Katika mahafali hiyo iliyojaa nuru, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa hotuba fupi na kuitaja kazi ya watu wanaojishughulisha na masuala ya Qur'ani katika kuiweka jamii ya Kiislamu karibu na Qur'ani na kuiongezea welewa na ufahamu wake pamoja na mapenzi makubwa kwa Qur'ani Tukufu, kuwa ni kazi muhimu sana na yenye thamani kubwa na ni kazi ya kiistratijia na ya kimsingi kabisa.
Amesema, inabidi kuwe na mipangilio mizuri kwa namna ambayo watu wa matabaka yote waweze kuwa karibu mno na Qur'ani kimaana, kimafunzo na kimapenzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Iwapo jamii ya Kiislamu itazidi kuwa na mapenzi na iwapo itazidi kuwa karibu na Qur'ani Tukufu siku baada ya siku, basi itaweza kuwa imara ndani kwa ndani na kwamba silaha ambayo inazipa nguvu jamii za wanadamu na kuwafanya washinde changamoto zote ni huko kuwa na uimara wa ndani kwa ndani jamii hizo.
Ametaja faida na baraka nyingine za kuwa na mapenzi na kuwa karibu mno na Qur'ani Tukufu kuwa ni kuimarika imani, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea ahadi za Mwenyezi Mungu pamoja na kuondokwa na hofu mbele ya matatizo ya kimaada na ya kidunia na kuongeza kuwa: Kuzingatia aya za Qur'ani Tukufu kunaifanya jamii ya Kiislamu kuwa mbali na kiza, na kuwa mbali na mambo ya upotofu, uzushi na kiza cha woga wa vitu visivyo na maana na kuielekeza jamii hiyo upande wa kumtambua Mwenyezi Mungu jambo ambalo leo hii ndicho kitu kikuu kinachohitajika zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kila namna.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameashiria suala la kuongezeka busuri, muono wa mbali na welewa wa umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Maadui wa Uislamu wanaogopeshwa mno na jambo hilo na ndio maana wanafanya njama za kutumia jina la Uislamu na vazi la Uislamu kukabiliana na dini tukufu ya Kiislamu.
Aidha amekumbushia istilahi iliyojaa hekima iliyotumiwa na Imam Khomeini ya kubainisha tofauti baina ya Uislamu wa Kimarekani na Uislamu asili wa Bwana Mtume Muhammad SAW akisisitiza kuwa: Hata kama Uislamu wa Kimarekani kijuu juu na katika dhahiri yake unaonekana kuwa na jina la Uislamu lakini unapatana na kuafikiana na taghuti na Uzayuni na unakubali kuwa chini ya mabeberu na kufuata amri za waistikbari na kimsingi unahudumia kikamilifu malengo ya taghuti na Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia ushahidi madhubuti na usiokanushika uliopo kuhusu kuhusika kikamilifu mashirika khabithi ya kijasusi ya adui katika fujo na machafuko yanayoshuhudiwa kwenye baadhi ya jamii za Waislamu kama vile Iraq na kuongeza kuwa: Kuwa karibu na kushikamana vilivyo na Qur'ani na kuweza umma wa Kiislamu kuwa na utambuzi wa kina kuhusu mafundisho ya Qur'ani Tukufu kutazuia mambo kama hayo kama ambavyo kutazuia pia usaliti wa baadhi ya watu kuhusu mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewataka watu wanaojihusisha na masuala ya Qur'ani Tukufu kulipa uzito wa hali ya juu suala la kushikamana vilivyo na mafundisho ya dini na kuongeza kwamba: Jamii iliyojaa fakhari ya Qur'ani Tukufu nchini Iran inapaswa kuwa kigezo na ruwaza njema ya kivitendo kwa vijana nchini.

1423909

captcha