IQNA

Waislamu Marekani walaani hujuma ya kigaidi Manhattan, New York

13:02 - November 01, 2017
Habari ID: 3471241
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Marekani wamelaani hujuma ya kigaidi iliyojiri Jumanne mjini New York katika mtaa wa Manhattan na kupelekea watu 8 kupoteza maisha.

Katika taarifa, Baraza la Marekani la Mahusiano ya Kiilamu, CAIR, limelaani hujuma hiyo na kutuma salamu za rambi rambi kwa wale ambao wamepoteza jamaa zao katika tukio hilo.

CAIR imesema lengo la ugaidi kama huo ni kuligawa taifa la Marekani na kwa msingi huo Wamarekani wa dini zote wanapaswa kuungana kukabiliana na ugaidi.

Watu wasiopungua wanane wameuawa na wengine kujeruhiwa baada ya gari kuingia kwa mwendo wa kasi katika njia ya waendao kwa miguu na wapanda baiskeli katika jiji la New York huko Marekani.

Tukio hilo lilijiri jana katika kitongoji cha Manhattan wakati gari aina ya pick-up lilipoingia kwa mwendo wa kasi katika njia ya waendao kwa miguu na wapanda baiskeli katika barabara kuu ya West Side na kuwagonga waendesha baiskeli kadhaa karibu na eneo la kumbukumbu la Jengo la Kimataifa la Biashara. Watu walioshuhudia wamesema kuwa miili ya wahanga imeshuhudiwa ikiwa imetapakaa chini nje ya shule ya serikali ya Stuyvesant na kwamba walisikia pia milio ya risasi tisa au kumi.

Uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa mshukiwa wa shambulio hilo la Manhattan ni Sayfullo Habibullaevic Saipov raia wa Uzbekistan mwenye umri wa miaka 29 ambaye alifika Marekani mwaka 2010 na alikuwa akiishi katika jimbo la Florida.

3464307

captcha