IQNA

Wakimbizi Waislamu Warohingya 300 wafika Indonesia baada ya miezi saba baharini

22:04 - September 07, 2020
Habari ID: 3473147
TEHRAN (IQNA) – Wakimbizi 300 Warohingya wamewasilia Indonesia mapema Jumatatu na kusema wamekuwa baharini kwa muda wa miezi saba.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema wakimbizi hao, wakiwemo watoto zaidi  ya 12, walionekana baharini wakiwa ndani ya boti ya mbao na kusaidiwa na wenyeji kufika karibu na mji wa Lhokseumawe katika kaskazini mwa pwani ya kisiwa cha Sumatra.

Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Indonesia Bi. Oktina, ambaye sawa na Waiondonesia wengi ana jina moja, amesema kwa mujibu wa ushuhuda uliotolewa na wakimbizi hao, wamekuwa baharni kwa muda wa miezi saba baada ya boti yao kuharibika na kupoteza dira. Amesema wakimbizi hao walikuwa dhaifu mno wakati walipowasili.

Hayo yanajiri siku chache zilizopita, - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa kutatuliwa tatizo la mgogoro wa wakimbizi Warohingya kupitia utatuzi wa chanzo kikuu cha sababu za wao kukimbia makazi yao nchini Myanmar.

Wiki iliyopita  Waislamu Warohingya ambao ni wakimbizi nchini Bangladesh walishiriki katika 'maandamano ya kimya kimya' kukumbuka mwaka wa tatu tokea waanze kufurushwa makwao nchini Myanmar.

Miaka mitatu iliyopita, yaani Agosti 2017, inadaiwa kuwa wanamgambo walishambulia vituo vya polisi na kituo cha kijeshi katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo maafisa 12 wa usalama waliuawa.

Jeshi la Myanmar lilitumia kisingizio hicho kuanzisha oparesheni kubwa ya maangamizi ya umati dhidi ya Waislamu Warohingya ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakandamizwa na kubaguliwa. Tukio hilo lilipelekea Warohingya 730,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh na kujiunga na wenzao laki mbili ambao katika miaka ya nyuma walikuwa wameikimbia nchi yao. Warohingya wengine pia wamekimbilia katika nchi kama vile Pakistan, India, Thailand, Malaysia na Indonesia.

Umoja wa Mataifa umesema ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar ambao unatekelezwa na jeshi la nchi hiyo una lengo la maangamizi ya kimbari.

3472490

captcha