Ayatullah Seyyed Ahmad Khatami, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesisitiza katika hotuba zake juu ya kufuatiliwa suala la wanafunzi kupewa vidhurishi na kukabiliana na wahusika wa suala hilo; na akatilia mkazo mwongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na haja ya kufuatiliwa suala la wanafunzi kupewa sumu na kuchukuliwa hatua waliohusika na akasema: Idara ya Mahakama inapaswa kuwachukulia hatua kali pia wale wanaoeneza uvumi kuhusiana na suala hilo kwenye mitandao ya intaneti au katika maandiko yao.
Ayatullah Khatami aliashiria malengo matatu ya maadui ya sumu hizi na akasema: "Lengo la kwanza ni kuharibu usalama. Hisia ya usalama ni muhimu zaidi kuliko usalama yenyewe. Akina baba na akina mama huwapeleka watoto wao shuleni na hadi saa sita mchana huwa na wasiwasi kuhusu lini watarudi, na hili ndilo lengo lao la kufanya wasiwasi huu uenee ulimwenguni kote. Lengo la pili ni kukomesha ukuaji wa kisayansi na kielimu wa watoto wa Iran."
Aidha amesema lengo la tatu kuwa ni shutuma dhidi ya mfumo wa Kiislamu na watu wanaofungamana na mafundisho ya Kiislamu kidini na akasema: "Uchongezi huu hakika ni dhambi kwa asilimia mia moja. Ikiwa vyombo vya habari vinatafuta uongo mkubwa katika siku za mwisho wa mwaka (wa Kiirani), ni kuandika tukio hili na kulaumu Mfumo wa Kiislamu na watu wanaofungamana na dini. Bila shaka, uwongo huu haujakubalika na hautakubaliwa."