IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /91

Mwenyezi Mungu Anaapa mara 11 katika Surah Ash-Shams

17:28 - July 03, 2023
Habari ID: 3477232
TEHRAN (IQNA) – Kuapa kwa kitu hutokea wakati suala muhimu sana litatajwa. Katika Surah Ash-Shams ya Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu anaapa mara 11 kabla ya kuashiria jambo muhimu sana.

Ash-Shams ni sura ya 91 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 15 na iko katika Juzuu ya 30.

Ni Makki na ni Sura ya 26 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Neno Shams (jua) linakuja mara 34 katika Qur'ani Tukufu, ikiwa ni pamoja na katika aya ya kwanza ya Sura hii inayoipa jina lake.

Mwenyezi Mungu anaapa mara 11 katika aya saba za kwanza za sura hii, idadi kubwa zaidi katika Sura yoyote ya Qur'ani Tukufu. Mwenyezi Mungu anaapa kwa jua, mwanga wa jua, mwezi unaofuata jua, mchana unaoangaza ardhi, usiku unapoifunika ardhi kwa giza, mbingu, aliyeiweka imara, ardhi, aliyeitandaza, nafsi, na Yeye aliyeifanya kuwa kamilifu.

Sababu ya viapo hivi kuja kimoja baada ya kingine ni kwamba suala muhimu sana litatajwa, jambo ambalo ni kubwa kama mbingu, ardhi, mwezi na jua. Imesemekana kwamba viapo ndani ya Qur'an vina malengo mawili: Kuangazia umuhimu wa kile anachoapa Mwenyezi Mungu, na kubainisha umuhimu wa somo lililotajwa baadaye.

Surah Ash-Shams inasisitiza usafi wa Nafs (nafsi) na inaiona kuwa ni njia ya kuokolewa ambapo ikiwa ni najisi inasababisha kupoteza matumaini. Aya hizo zinatukumbusha kwamba watu wanatofautisha kati ya mema na mabaya kulingana na utambuzi wao wa ndani waliopewa na Mungu, na kwamba tunapaswa kuitakasa nafsi zetu kwa kufanya matendo mema, vinginevyo hatutafikia furaha.

Sura imetoa mfano wa watu wa Thamud waliomuasi Mtume wao, Salih (AS), na wakamuua ngamia ambao ulikuwa ni muujiza wa Mwenyezi Mungu na hivyo wakaadhibiwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Hadith kutoka kwa Imamu Sadiq (AS), jua ni ishara ya Mtukufu Mtume (SAW) ambaye anaangazia dini, mwezi unaashiria Imam Ali (AS) ambaye (alipokea) elimu aliyokuwa nayo Mtukufu Mtume (SAW) usiku unaashiria watawala na wafalme madhalimu na mchana unaashiria viongozi wakuu wanaoangazia njia ya dini.

captcha