IQNA

Ifahamu Qur'ani Tukufu /12

Fadhila ya Qur'ani Tukufu kuwa katika Kiarabu

21:11 - July 04, 2023
Habari ID: 3477237
TEHRAN (IQNA) – Moja ya sifa ambazo Mwenyezi Mungu anaielezea Qur'ani Tukufu ni kwamba imeteremshwa kwa Kiarabu. Je, ni nini fadhila ya Quran kuwa katika lugha ya Kiarabu?

Ukweli kwamba Qur'ani Tukufu iko katika Kiarabu umetajwa katika aya kadhaa za Kitabu Kitukufu, na hii ni nukta ambayo inaashiria umuhimu wa kadhia hii. Aya hizo ni pamoja na aya ya 113 ya Surah Taha, aya ya 28 ya Surah Az-Zumar, aya ya 37 ya Surah Ar-Raad, na 12 ya Surah Al-Ahqaf.

Pia kuna Aya ya 2 ya Sura Yusuf: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia."

Wanafikra na wafasiri wa Qur'ani wametaja sababu tofauti za kutilia mkazo juu ya Qur'ani Tukufu kuwa katika Kiarabu.

Moja ni uwazi wa lugha ya Kiarabu. Ragheb Esfahani katika kitabu chake cha Falsafa ya Kiarabu anakichukulia Kiarabu kuwa ni lugha iliyo wazi na fasaha na anasema kuwa Qur'ani Tukufu katika Kiarabu inadhihirisha wazi ukweli na kubainisha uwongo.

Lugha ya Kiarabu inayozungumzwa huko Hijaz ina viwakilishi vingi vinavyotofautiana katika idadi na jinsia. Pia ina uwezo mwingi wa kuwasilisha maana kwa idadi ndogo ya maneno na kwa uwazi wa hali ya juu.

Ufasaha ni miongoni mwa vipengele vingine vinavyotofautisha lugha ya Kiarabu na lugha nyinginezo.

Zaidi ya hayo, ni Sunna ya Mwenyezi Mungu kwamba kila mjumbe wa Mwenyezi Mungu anatumwa kwa watu kuzungumza nao kwa lugha yao wenyewe. Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) aliteuliwa kuwa utume miongoni mwa Waarabu, hivyo kitabu kitakatifu alichoteremshiwa kikawa ni  katika Kiarabu.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 44 ya Surah Al-Fussialt: “Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.?"

Uchunguzi wa kihistoria wa lugha ya Kiarabu kabla na baada ya kuteremshwa Qur'ani Tukufu unaonyesha kwamba Waarabu walioishi kabla ya kuja Uislamu walijua kanuni nyingi za balagha na baadhi yao walikuwa wastadi sana kiasi cha kuhakiki mashairi na kubainisha udhaifu na nguvu zao.

Qur'ani Tukufu iliwataka kuleta Sura kama hiyo ya Qur'ani Tukufu lakini walishindwa kufanya hivyo na hakuna mtu mwingine yeyote tangu wakati huo aliyeweza kuifanya. Huu ni uthibitisho wa ufasaha wa Qur'ani Tukufu na ni sababu nzuri inayothibitisha kuwa ni kitabu kitakatifu.

captcha